Simba SC Yakaribia Kuachana na Kipa Ally Salim Licha ya Mkataba Wake Kumalizika 2027
Mlinda mlango wa klabu ya Simba SC, Ally Salim, ameripotiwa kuwa miongoni mwa wachezaji wanaotarajiwa kuondoka ndani ya klabu hiyo katika dirisha la usajili kuelekea msimu mpya wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Taarifa kutoka ndani ya klabu hiyo zinasema kuwa licha ya Salim kuwa na mkataba unaomalizika mwaka 2027, hayumo kwenye mipango ya benchi la ufundi kwa msimu ujao. Hali hiyo imeibua mjadala juu ya hatma ya kipa huyo ambaye aliwahi kuwa sehemu muhimu ya kikosi cha Simba, hasa katika nyakati ambazo kikosi hicho kilikuwa kinapambana kwenye mashindano ya ndani na ya kimataifa.
Kumekuwa na tetesi kuwa Simba inaweza kuchukua uamuzi wowote kuhusu Salim, ikiwemo kumuuza kwa timu nyingine au kuvunja mkataba wake kwa makubaliano maalum. Tayari baadhi ya klabu za Ligi Kuu zimeonyesha nia ya kumsajili mlinda mlango huyo ambaye ana uzoefu na rekodi nzuri ndani ya ligi ya Tanzania.
Salim alijiunga na kikosi cha kwanza cha Simba mwaka 2018 akitokea timu ya vijana ya Simba B. Tangu wakati huo, akiwa na kikosi hicho, Simba imefanikiwa kutwaa mataji manne ya Ligi Kuu Bara katika misimu ya 2017/18, 2018/19, 2019/20 na 2020/21.
Endapo uamuzi huo utatekelezwa, Ally Salim atakuwa mmoja wa majina makubwa kuondoka Msimbazi katika kipindi hiki cha mabadiliko makubwa ndani ya kikosi cha Simba SC.
Post a Comment
Post a Comment