
Ligi Kuu ya Wanawake Tanzania Bara (WPL) msimu wa 2026/27 inaanza leo Jumatano, Oktoba 28, 2026, kwa mechi sita za raundi ya kwanza zitakazochezwa kwenye viwanja sita tofauti nchini. Mechi zote zimepangwa kuanza saa 10:00 jioni.
Timu 12 zinashiriki msimu huu, zikiwemo Kilimanjaro Wonders na Bunda Girls zilizopanda daraja kutoka ligi za mkoa. Mabingwa watetezi Simba Queens wanaanzia ugenini mkoani Kilimanjaro, huku JKT Queens, waliomaliza nafasi ya pili msimu uliopita, wakisafiri hadi Geita.
Ratiba ya Ligi Kuu ya Wanawake Leo
Hizi ndizo mechi za ufunguzi wa msimu, zote zikianza saa 10:00 jioni:
Fountain Gate Princess Vs Mashujaa Queens
Uwanja wa Jamhuri, Dodoma
Kilimanjaro Wonders Vs Simba Queens
Uwanja wa Ushirika, Moshi
Bunda Girls Vs Yanga Princess
Uwanja wa Karume
Geita Queens Vs JKT Queens
Uwanja wa Nyankumbu, Geita
Ceasiaa Queens Vs Alliance Girls
Uwanja amora, Iringa
Tausi FC Vs Bunda Queens
Uwanja wa Nyamagana, Mwanza
Somoe: Huu Utakuwa Msimu Bora Zaidi
Mwenyekiti wa Chama cha Soka la Wanawake Tanzania, Somoe Ng'itu, ambaye pia ni mjumbe wa Kamati Tendaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), amesema msimu huu unatarajiwa kuwa na ushindani mkubwa kuliko iliyopita.
"Tumetembelea kila timu kuangalia maandalizi yao na hakika kwa kiasi kikubwa tumejiridhisha na matayarisho yao, yataleta ushindani mkubwa sana," alisema Somoe kupitia taarifa iliyotolewa na TFF jana.
Kwa mujibu wa kiongozi huyo, ishara za ushindani huo zilionekana tayari kwenye mechi tatu za Ngao ya Jamii 2026. Ameongeza kuwa mashabiki wameendelea kujitokeza viwanjani kuziunga mkono mechi za ligi hiyo, jambo linaloonyesha kukua kwa soka la wanawake nchini.
JKT Queens Kuanza Vita ya Kurejesha Taji Geita
JKT Queens ndiyo timu pekee iliyoweza kushindana bega kwa bega na Simba Queens katika misimu ya karibuni. Wanajeshi hao walitwaa ubingwa msimu wa 2024/25, lakini msimu uliopita walimaliza wa pili nyuma ya Simba Queens.
Walianza maandalizi ya msimu kwa kufika fainali ya Ngao ya Jamii, ambako walipoteza kwa bao 1-0 dhidi ya Simba Queens Oktoba 3, 2026. Leo wanaanza safari ya kurejesha taji dhidi ya Geita Queens kwenye Uwanja wa Nyankumbu.
Yanga Princess, waliomaliza nafasi ya tatu msimu uliopita, bado wanasaka taji lao la kwanza la WPL. Wanaanza dhidi ya Bunda Girls, timu iliyopanda daraja na inayocheza ligi kuu kwa mara ya kwanza.
Timu Mpya na Dabi za Kufuatilia Msimu Huu
Kilimanjaro Wonders wanaingia kwenye ligi kuu kwa mara ya kwanza katika historia yao, na mtihani wao wa kwanza ni dhidi ya mabingwa watetezi kwenye Uwanja wa Ushirika, Moshi. Ni nafasi kwa timu hiyo kujitambulisha mbele ya mashabiki wake.
Bunda Girls nao wanaleta dabi mpya ya Kanda ya Ziwa, kwa kuwa msimu huu watakutana na Bunda Queens, timu inayotoka eneo moja. Leo Bunda Queens wanaanzia ugenini dhidi ya Tausi FC jijini Mwanza.
Dabi nyingine inayosubiriwa ni ya timu za kijeshi kati ya Mashujaa Queens na JKT Queens. Katika mikutano minne iliyopita, Mashujaa haijawahi kuifunga JKT, ambayo imeshinda mara tatu na kutoka sare mara moja. Mashujaa Queens wanaanza msimu leo dhidi ya Fountain Gate Princess jijini Dodoma.
Huko Iringa, Ceasiaa Queens watakuwa wenyeji wa Alliance Girls kwenye Uwanja wa Samora. Matokeo ya raundi hii ya kwanza yatatoa picha ya kwanza ya msimamo wa Ligi Kuu ya Wanawake 2026/27.
Soma pia
Kombe la Shirikisho: Azam Kapu la Pili, Singida Kapu la Tatu
Msimamo wa Ligi Kuu NBC 27 Oktoba: Yanga Yapunguza Pengo Hadi 2
Liverpool vs Chelsea Leo 28 Oktoba 2026 na Azam vs Mbeya City